Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni ndg. Stephen Katemba ametoa agizo la kufungwa kwa shule zote za Awali,Msingi na Sekondari za binafsi zisizo na usajili na zile zenye mazingira hatarishi kwa wanafunzi.
Zoezi hilo lililoanza leo tarehe
22 Agosti 2017 limepanga kufunga shule 58 za awali na msingi ambazo mpaka sasa
zimebainika kutokuwa na usajili wa aina yoyote huku zikiendelea kutoa elimu
pamoja na kuwa walishapewa barua toka Januari 2017 ikiwataka kutopokea
wanafunzi mpaka hapo watakapokamilisha usajili.
Ofisi ya Afisa elimu Manispaa ya
Kigamboni ikishirikiana na wakaguzi wa ubora wa elimu ilipewa jukumu la kupita
shule hadi shule na kuzifunga kwa niaba ya Mkurugenzi endapo zitakuwa hazijakidhi
vigezo vya kutoa elimu.
Msimamizi wa zoezi hilo Kaimu
Afia elimu Msingi Mwl. Mathew Komba alisema zoezi hili litaendelea kwa siku
tano mfululizo ambapo kwa siku ya kwanza zoezi lilifanyika katika kata tatu za
Vijibweni,Kigamboni na Tungi ambapo shule 18 zilifungwa na wamiliki wa shule
hizo kutakiwa kusimamisha zoezi la ufundishaji kuanzia leo tarehe 22 Agosti na
endapo watakaidi hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Baadhi ya shule zilizofungwa ni
pamoja na shule ya awali ya Malaika, Kigamboni English Medium school, Patmos
,Montecalos pamoja na Riziki. Zingine ni Taqwa ,Fildaus ,Mek na Charity.
Mkurugenzi wa Manispaa ya
Kigamboni Ndg Stephen Katemba anatoa wito kwa wamiliki wote waliofungiwa shule
kutojaribu kufungua shule hizo mpaka hapo ofisi yake itakaporidhika kulingana
na maagizo yaliyotolewa.
kaimu Afisa Elimu Msingi Mwalimu Mathew Komba (Katikati) akimpa maelekezo mmiliki wa shule ya Malaika iliyopo kata ya Tungi |
Wanafunzi wakiwa wamelala katika mazingira yasiyokubalika na muongozo wa usajili wa shule |
Baadhi ya wanafunzi wa Kigamboni Islamik Nursery and Primary school wakifundishwa katika jengo la Msikiti badala ya darasani |