Jumatano, 6 Desemba 2017

TBA KUJENGA OFISI ZA MANISPAA








Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni Ndg. Stephen Katemba pamoja na Mtendaji mkuu wa wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Ndg Eliud Mwakalinga wametia saini ya mkataba wa ujenzi wa ofisi ya Halmashauri ya Manispaa kuanzia Januari 2018.Ujenzi huo wa ofisi unatajiwa kuchukua miezi Minane na unatarajiwa kukamilika mwezi wa tisa mwaka 2018.

Kukamilika kwa ujenzi huo kutaondoa usumbufu kwa watumishi na wananchi wanaofika kupata huduma kutokana na ofisi za Idara mbali mbali kuwa sehemu tofauti tofauti  hivyo kuwalazimu wananchi na watumishi kusafiri toka ofisi moja kwenda nyingine.
Kwa upande wa rasilimali ,Halmashauri itaokoa zaidi ya shilingi milioni 30 zinazotumika kulipia ofisi za Manispaa katika majengo ya watu binafsi kwa Mwaka.Mtendaji mkuu wa TBA Ndg. Mwakalinga alimuhakikishia Mkurugenzi kuwa wanakabidhi jengo kwa muda waliokubaliana kwenye mkataba.

 

Jumatano, 11 Oktoba 2017

PIMA AFYA BURE

Mkurugenzi wa Halmashauri anawakaribisha wananchi wote kufika katika viwanja vilivyopo karibu na ofisi za Halmashauri kuanzia tarehe 10/10/2017 hadi 15/10/2017 kwa ajili ya kupima afya. Huduma zitolewazo ni pamoja na kupima maambukizi ya virusi vya ukimwi, shinikizo la damu,Kisukari, Saratani kwa akina mama/baba (Huduma inatolewa katika Hospitali ya Vijibweni) na Tezi dume.(Huduma inatolewa katika Hospitali ya Vijibweni)


 KARIBUNI SANA.

WAKAZI WA KIGAMBONI WAKIPATIWA HUDUMA





KARIBUNI SANA KUWEKEZA KIGAMBONI

Wageni mbalimbali wameendelea kumiminika kwa ajili ya kuwekeza katika Halmashauri yetu. Karibuni sana wote kwani Tanzania ya viwanda kigamboni inawezekana.

Mkurugenzi wa Halmashauri Bw. Stephen E. Katemba (katikati) akiwa na wawekezaji

MAFUNZO YA PLANREP

Wakuu wa Idara/ Vitengo na Maafisa Bajeti wamepewa mafunzo juu ya utumiaji wa mfumo mpya wa uandaaji wa bajeti (PLANREP) ya Halmashauri na Mkufunzi wa ndani Bw. Masore Masogo - Mtakwimu Mkuu.





Ijumaa, 29 Septemba 2017

MSAADA KWA WAZEE

Mkurugenzi Mkazi wa shirika la World Share la nchini Korea Nara Kim (wanne kutoka kulia) kwenye picha ya pamoja na uongozi wa kituo cha kulelea wazee Nunge walipofika kutoa msaada wa vitu mbalimbali.

BARAZA MAALUMU LA KUPITIA TAARIFA YA UFUNGAJI WA HESABU UNAOISHIA 30 JUNI

Mkutano Maalumu wa Baraza la Madiwani ukiongozwa na Mstahiki Meya Maabad Suleiman Hoja kwa ajili ya  kupitisha  taarifa ya ufungaji wa Mahesabu kwa mwaka unaoishia 30 Juni 2017










Mkurugenzi Bw. Stephen E. Katemba (aliyesimama) akiwasilisha agenda

Viongozi wa Halmashauri wakifuatilia agenda mbalimbali kwa umakini


Waheshimiwa Madiwani wakisikiliza uwasilishaji wa Agenda tayari kwa kuchangia

Mhe. Sanya Bunaye Diwani wa Kata ya Kimbiji (wakwanza kulia) akichangia mada katika mkutano wa baraza


Jumanne, 22 Agosti 2017

MKURUGENZI AFUNGA SHULE 18 ZISIZOSAJILIWA


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni ndg. Stephen Katemba ametoa agizo la kufungwa kwa shule zote za Awali,Msingi na Sekondari za binafsi zisizo na usajili na zile zenye mazingira hatarishi kwa wanafunzi.


Zoezi hilo lililoanza leo tarehe 22 Agosti 2017 limepanga kufunga shule 58 za awali na msingi ambazo mpaka sasa zimebainika kutokuwa na usajili wa aina yoyote huku zikiendelea kutoa elimu pamoja na kuwa walishapewa barua toka Januari 2017 ikiwataka kutopokea wanafunzi mpaka hapo watakapokamilisha usajili.

Ofisi ya Afisa elimu Manispaa ya Kigamboni ikishirikiana na wakaguzi wa ubora wa elimu ilipewa jukumu la kupita shule hadi shule na kuzifunga kwa niaba ya Mkurugenzi endapo zitakuwa hazijakidhi  vigezo vya kutoa elimu. 

Msimamizi wa zoezi hilo Kaimu Afia elimu Msingi Mwl. Mathew Komba alisema zoezi hili litaendelea kwa siku tano mfululizo ambapo kwa siku ya kwanza zoezi lilifanyika katika kata tatu za Vijibweni,Kigamboni na Tungi ambapo shule 18 zilifungwa na wamiliki wa shule hizo kutakiwa kusimamisha zoezi la ufundishaji kuanzia leo tarehe 22 Agosti na endapo watakaidi hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Baadhi ya shule zilizofungwa ni pamoja na shule ya awali ya Malaika, Kigamboni English Medium school, Patmos ,Montecalos pamoja na Riziki. Zingine ni Taqwa ,Fildaus ,Mek na Charity.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni Ndg Stephen Katemba anatoa wito kwa wamiliki wote waliofungiwa shule kutojaribu kufungua shule hizo mpaka hapo ofisi yake itakaporidhika kulingana na maagizo yaliyotolewa.



kaimu Afisa Elimu Msingi Mwalimu Mathew Komba (Katikati) akimpa maelekezo mmiliki wa shule ya Malaika iliyopo kata ya Tungi

Wanafunzi wakiwa wamelala katika mazingira yasiyokubalika na muongozo wa usajili wa shule

Baadhi ya wanafunzi wa Kigamboni Islamik Nursery and Primary school  wakifundishwa katika jengo la Msikiti badala ya darasani

Jumatatu, 21 Agosti 2017

MALIPO YOTE KWA MASHINE YA EFD

Vijana wa Kigamboni wakionesha utaalamu wao wa kutumia mashine ya EFD kwa viongozi wa Wilaya hiyo. Kutoka kulia ni Mkuu wa Wilaya  Mhe. Hashim Mgandilwa na Mkurugenzi Bw. Stephen Katemba



Mkuu wa Wilaya Mhe. Hashim Mgandilwa akiangalia risiti iliyochapishwa kwa mashine ya EFD kama inakidhi mahitaji ya Halmashauri na kuitambulisha kwa ufasaha.

Mkuu wa Wilaya Mhe. Hashim Mgandilwa akionesha mfano wa risiti ya mashine ya EFD ambayo itatumika kwa malipo yote katika Halmashauri

Vijana wanaweza. Viondozi wa Halmashauri(waliovaa t-shirt za rangi ya kijani kibichi wakiangalia kama vijana wanaweza kutumia mashine za EFD kwa ufasaha

Jumapili, 20 Agosti 2017

USAFI KWANZA

Wananchi wa Kigamboni mnatakiwa kufanya usafi kuzunguka maeneo yenu ya makazi na biashara. Ukaguzi utaendelea kufanyika na endapo eneo lako litakuwa chafu, hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwemo faini za papo kwa papo.

Vijana wa Kigamboni wakiwa tayari kuingia msituni kupambana na adui takataka. Kigamboni safi ya mfano inakuja

Alhamisi, 3 Agosti 2017

KARIBU KATIKA BANDA LETU MOROGORO

Karibuni sana katika banda letu la maonesho lililopo katika viwanja vya Nane Nane Mkoani Morogoro. Katika banda hili mtajifunza ukulima wa kisasa, ufugaji wa kisasa kwa mifugo ya aina zote na njia mpya za Kilimo biashara na kutambua maeneo ya uwekezaji.

Karibuni sana, sana.


Mstahiki Meya Maabad Suleiman Hoja (Katikati) akiwa na Naibu Meya Mhe. Amin Mzuri Sambo(kulia) na Mkurugenzi Bw. Stephen Katemba
 

Jumatatu, 31 Julai 2017

VITUO VYA AFYA VYAPATA ALAMA ZA JUU

Mkurugenzi Bw. Stephen Katemba (kulia) akipokea taarifa kutoka kwa Bi. Ruth Ngowi          





Katika ukaguzi wa Kimaabara uliofanywa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka 2017 ,Vituo vya Afya katika Manispaa ya Kigamboni vimeonekana kuwa na alama za juu katika kutoa huduma kwa Jamii.
Katika kaguzi huo ulioongozwa na Bi.Ruth Ngowi,Jumla ya vituo vya Afya 13 vimepata alama za nyota Tatu  na zaidi ikiwa ni kiashiria kuwa huduma zinazotolewa ni bora na za kuridhisha.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni alikabidhiwa ripoti hiyo na timu ya ukaguzi na kuahidi kuendelea kusimamia ubora zaidi kwani kwa upande wa vituo vya Afya vilivyo chini yake vilikuwa na alama 76 tofauti na alama za jumla za 48 inayounganisha vituo vya serikali na vya Binafsi.
Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni ina Jumla ya Vituo vya Afya 27,kati ya hivyo 17 ni vya serikali na 10 ni vya watu binafsi na mashirika mbali mbali.

Picha ya pamoja ya watumishi wa Halmashauri na Wizara

Alhamisi, 27 Julai 2017

WAZEE 2376 WAPATIWA VITAMBULISHO VYA MATIBABU BURE




Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy  Ally Mwalimu

Waziri wa Afya ,Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,wazee na watoto Mh. Ummy Mwalimu amekabidhi zaidi ya vitambulisho 2300 kwa wazee wa Manispaa ya Kigamboni kwa ajili ya kuwawezesha kupata matibabu bila malipo katika hospitali zote za Manispaa ya Kigamboni.

Zoezi la utoaji vitambulisho hivyo limefanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Kigamboni ( Vijibweni) na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa manispaa ya kigamboni wakiongozwa na mkuu wa Wilaya Mh. Hashim Mgandilwa.

Viongozi wengine waliohudhurio hafla hiyo ni pamoja na Meya wa manispaa ya Kigamboni Mh.Maabad Suleiman Hoja ,Waheshimiwa madiwani pamoja na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni ndg Stephen Katemba.

Akisoma risala mbele ya mgeni Rasmi Ndg Katemba alisema wazee hao 2376 ni sehemu ya wazee 7000 wanaotarajiwa kunufaika na mpango huo kwani mpaka sasa zoezi la kuwatambua linaendelea chini ya usimamizi wa idara ya Ustawi na maendeleo ya Jamii wa Manispaa ya Kigamboni.

Mkurugenzi aliongeza kuwa ,kuanzia sasa hatarajii kuona wazee wakipata tabu ya matibabu kwani mpango huo unawawezesha kupata matibabu yote bure kuanzia vipimo mpaka kumuona Daktari.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy  Ally Mwalimu akimkabidhi kitambulisho cha matibabu Mzee Jafary Said Said.


Picha ya pamoja
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy  Ally Mwalimu akiongea na wananchi

















Jumatano, 26 Julai 2017

NAFASI ZA KAZI



Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni imepokea kibali Kumb. Na. FA 170/374/01/27 cha tarehe 14 Julai, 2017 kutoka kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Kibali Kumb. Na. FA.102/282/02B/13 cha tarehe 30 Juni, 2017 kutoka kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni anawatangazia wananchi wote raia wa Tanzania wenye sifa kuomba nafasi zilizoorodheshwa hapo chini.

1.     MTENDAJI WA MTAA DARAJA LA III-  (NAFASI 31)
(a)   Sifa za Mwombaji
Kuajiriwa mwenye Elimu ya Kidato cha Nne (IV) au Sita (VI) aliyehitimu mafunzo ya Astashahada/Cheti katika moja ya fani zifuatazo: Utawala, Sheria, Elimu ya Jamii, Usimamizi wa Fedha, Maendeleo ya Jamii na Sayansi ya Sanaa kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, Dodoma au Chuo chochote kinachotambuliwa na Serikali.
Kazi na majukumu ya Mtendaji wa Mtaa
(a)   Katibu wa kamati ya Mtaa
(b)   Mtendaji Mkuu wa Mtaa
(c)   Mratibu wa utekelezaji wa Sera na Sheria zinazotekelezwa na Halmashauri katika Mtaa
(d)   Mshauri wa Kamati ya Mtaa kuhusu Mipango ya Maendeleo katika Mtaa
(e)   Msimamizi wa Utekelezaji wa Sheria ndogo pamoja na Sheria nyingine zinazotumika katika Mtaa
(f)    Mshauri wa Kamati ya Mtaa kuhusu masuala ya Ulinzi na Usalama
(g)   Msimamizi wa utekelezaji wa mikakati mbalimbali inayohusu uondoaji wa njaa na Umaskini katika Mtaa
(h)   Kusimamia ukusanyaji wa Mapato ya Halmashauri na kutunza kumbukumbu za walipa kodi wote
(i)     Kuandaa na kutunza rejesta ya wakazi wote wa Mtaa
(j)     Atawajibika kwa Mtendaji wa Kata

       Ngazi ya mshahara ni TGS B sawa na Shilingi 390,000/= kwa mwezi

2.     MTUNZA KUMBUKUMBU MSAIDIZI DARAJA LA II  (NAFASI 5)
(a)   Kuajiriwa mwenye Elimu ya Kidato cha Nne (IV) au cha Sita (VI) waliohudhuria mafunzo ya Utunzaji wa Kumbukumbu nakupata cheti cha NTA LEVEL 5 katika mojawapo ya fani za Afya,Masjala, Mahakama na Ardhi

Kazi na Majukumu
(a)   Kutafuta kumbukumbu/nyaraka/mafaili yanayohitajiwa na wasomaji
(b)   Kudhibiti upokeaji, uandikishaji wa kumbukumbu/ nyaraka
(c)   Kuweka/kupanga kumbukumbu/nyaraka katika reki (file racks/cabinets) katika masjala/vyumba vya kuhifadhia kumbukumbu
(d)   Kuweka kumbukumbu (barua,nyaraka n.k) katika mafaili
(e)   Kushughulikia maombi ya kumbukumbu/nyaraka kutoka Taasisi za Serikali

          Ngazi ya mshahara ni TGS B sawa na Shilingi 390,000/= kwa mwezi

3.     KATIBU MAHSUSI DARAJA LA III   (NAFASI 1)
(a)   Kuajiriwa mwenye Elimu ya Kidato cha Nne (IV) waliohudhuria mafunzo ya Uhazili nakupata cheti cha NTA LEVEL 5. Wawe wamefaulu somo la hati mkato ya Kiswahili na Kiingereza maneno 80 kwa dakika moja na wawe wamepata mafunzo ya kutumia kompyuta kutoka Chuo chochote kinachotambuliwa na Serikali nakupata Cheti katika programu za Windows,Microsoft Office,Internet,E-mail na Publisher.

     KAZI NA MAJUKUMU YA KATIBU MAHSUSI DARAJA LA III  
(a)   Kuchapa barua, taarifa na nyaraka za kawaida
(b)   Kusaidia kupokea wageni na kuwasaili shida zao, na kuwaelekeza sehemu wanapoweza kushughulikiwa
(c)   Kusaidia kutunza taarifa/kumbukumbu za matukio, miadi, wageni, tarehe za vikao, safari za mkuu wake na ratiba za kazi nyingine zilizopangwa kutekelezwa katika Ofisi anayofanyia kazi na kumuarifu mkuu wake kwa wakati unaohitajika
(d)   Kusaidia kutafuta na kumpatia Mkuu wake majalada, nyaraka au kitu chochote kinachohitajika katika shughuli za hapo Ofisini
(e)   Kusaidia kufikisha maelekezo ya Mkuu wake wa kazi kwa wasaidizi wake na pia kumuarifu kuhusu taarifa zozote anazokuwa amepewa na wasaidizi hao
(f)    Kusaidia kupokea majalada, kuyagawa kwa Maofisa walio katika Sehemu alipo, na kuyakusanya, kuyatunza na kuyarudisha sehemu zinazohusika
(g)   Kutekeleza kazi zozote atakazokuwa amepangiwa na Msimamizi wake wa kazi

    Ngazi ya mshahara ni TGS B sawa na Shilingi 390,000/= kwa mwezi

4.     MSAIDIZI WA HESABU     (NAFASI 2)
(a)   Kuajiriwa wenye Cheti cha ATEC level II au “Foundation Level” kinachotambuliwa na NBAA, waombaji wawe na uzoefu wa kazi zaidi ya mwaka (1) katika fani hiyo

  KAZI NA MAJUKUMU YA MSAIDIZI WA HESABU.
(a)   Kuandika na kutunza “register”zinazohusu shughuli za uhasibu
(b)   Kuandika hati za malipo na hati za mapokezi ya fedha
(c)   Kutunza majalada yenye kumbukumbu za hesabu
(d)   Kupeleka barua/ nyaraka za Uhasibu benki Kufanya usuluhisho wa masurufu, karadha, Hesabu za Benki na Amana.

Ngazi ya mshahara ni TGS B sawa na Shilingi 390,000/= kwa mwezi

NB. Kwa nafasi ya Msaidizi wa Hesabu itakuwa ni kwa Mkataba wa Mwaka mmoja na waombaji wawe tayari kufanya kazi katika Vituo vya Afya.

MASHARTI KWA UJUMLA
1.     Mwombaji awe raia wa Tanzania na awe tayari kufanya kazi sehemu yoyote ya Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni
2.     Mwombaji awe na Umri usiozidi miaka 45 na awe hajawahi kupatikana na kosa lolote la jinai, kufungwa jela au kufukuzwa kazi katika Utumishi wa Umma
3.     Waombaji  waambatishe maelezo yao binafsi (C.V)
4.     Maombi yote yaambatane na nakala ya vyeti vya taaluma, vyeti vya kidato cha (IV au VI), cheti cha kuzaliwa na picha mbili za rangi za hivi karibuni na ziandikwe majina nyuma
5.     “Testemonials, provisional results, Statment of Results hati ya matokeo ya kidato cha nne na sita (FORM IV and FORM VI RESULT SLIPS) HAVITAKUBALIWA
6.     Waombaji waliosoma nje ya Tanzania wahakikishe vyeti vyao vimehakikiwa na kuidhinishwa na Mamlaka husika TCU na NACTE na taarifa ya uhakiki iambatishwe kwenye maombi
7.     Uwasilishwaji wa taarifa na sifa za kugushi wahusika watachukuliwa hatua za kisheria
8.     Barua zote za maombi ziandikwe kwa mkono
9.     Mwisho wa kupokea barua za Maombi ni tarehe 15.08.2017 saa 9:30 alasiri.

Maombi yatumwe kwa Anuani ifuatayo:

Mkurugenzi,
Halmashauri ya Manispaa Kigamboni,
S.L.P 36009,
Kigamboni, Dar es Salaam.